AD (728x90)

Friday, October 28, 2011

Kanisa la Moravian lawakumbuka yatima

Yatima wakipokea misaada
Peter Edson
KANISA la Moravian Jimbo la Misheni Mashariki,  juzi liliandaa hafla ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu,  ambapo zaidi ya watoto 200 walihudhuria na kuzawadiwa vitu mbalimbali.Akifungua hafla hiyo iliyofanyika katika kanisa hilo ushirika wa Kinondoni jijini Dar es Salaam Makamu Mwenyekiti wa jimbo hilo Mch Saul Kajura alisema kushuka kwa maadili, na kupungua kwa uaminifu katika ndoa ni moja ya sababu zinazosababisha kuendelea kuongezeka kwa yatima na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
 Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo viongozi wa dini, Jamii  na Serikali hawana budi kuongeza jitihada za kukabiliana na ongezeko hilo kwa kudhibiti mianya ya ufujaji wa fedha za misaada zinazotolewa kwa ajili ya kuwatunza watoto hao ikiwa ni pamoja na kufundisha jamii ili iweze kuishi katika maadili mema.

 "Kama kanisa tunashukuru kwa kuwa Serikali inaonyesha jitihada kubwa sana za kukabiliana na jambo hili, sisi tunaamini kuwa kama jamii ikibadilisha mtizamo kwa kulinda na kuheshimu ndoa zao, pia Serikali ikidhibit ufujaji wa fedha za misaada kwa watoto hawa , tutapunguza kwa asilimia kubwa suala hili." alisema Mch. Kajura.

Alisema Mara nyingi taasisi binafsi zinazofanya kazi ya kulea na kuwatunza watoto hao zimekuwa zikitoa taaarifa ambazo si sahihi jambo ambalo kwa namna moja limekuwa likipotosha jitihada za makusudi zinazofanywa na Serikali katika kudhibiti ongezeko hilo.

Alisema kwa pamoja viongozi wa dini na Serikali wakiwekeza katika kukemea maovu mbalimbali ambayo ni chanzo kikubwa cha uzalishaji wa watoto hawa wanaweza kupungua kwa kiwango kikubwa.

Naye kiongozi wa kitengo cha ustawi wa jamii jimboni humo Phoibe Mwaipopo alisema,  kwa sasa jimbo hilo linahudumia watoto 200 wanaoishi katika mazingira magumu na kwamba mradi huo ulianza mwaka 2007.

Alisema watoto hao wamekuwa wakihudumiwa majumbani mwao kwa kutoa huduma za vyakula kuwasomesha kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba chini ya uangalizi wa maafisa  ustawi wa jamii katika kanisa hilo.

Alisema upungufu wa fungu la kuendeshea mradi huo  umekuwa chanzo cha kutofanya vizuri hivyo alitoa wito kwa wananchi na watu wenye mapenzi mema kujitokeza ili waweze kuwasaidia watoto hao kwa namna moja ama nyingine.

Hafla hiyo za watoto yatima ilifanyika juzi katika kanisa la Moravian Ushirika wa Kinondoni ambapo watoto waliweza kupata zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwazawadia watoto waliofanya vizuri katika masomo yao katika shule wanazotoka.

Mwisho.

No comments:

© 2013 HEKIMA KWAYA MORAVIAN-KINONDONI . All rights resevered. Designed by Templateism