AD (728x90)

Thursday, June 9, 2011

Waabuduo halisi watamuabudu Mungu katika roho na kweli.

Utaungana nami kuwa kusifu na kuabudu ni nguzo imara katika imani yetu ya kikristo kwani humfanya mkristo ajiweke tayari kwa kupokea zawadi ya ishara ya ukamilifu kutoka Mbinguni lakini pia humuondoa mtu kutoka katika hali  fulani ya kidunia na akajikuta akitizama yaliyo juu kwani imeandikwa waabuduo halisi watamuabudu Mungu katika roho na kweli.

Yawezekana mwimbaji ama mkristo  umekuwa ukijishusha na kujiona kuwa huna thamani mbele za Mungu jambo ambalo si kweli, wewe ni wa thamani sana kinachohitajika hapa ni wewe kubadili mtizamo na kuchukua hatua ya kumwabudu Mungu wetu aliye mbunguni kwa roho na kweli.


Katika hili tunaweza kuona yule mwanamke akamwambia [Yesu], ‘Bwana, naona ya kuwa u nabii. Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.’ Yesu akamwambia, ‘Mama, unisadiki. Saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu wala kule Yerusalemu. … Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana, Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli’ (Yohana 4:19-24).

Maneno hayo kutoka kinywa cha Yesu yanaweka msingi wa sisi kuelewa juu ya mambo muhimu sana katika kuabudu. Yeye alizungumzia juu ya “waabuduo halisi” na kueleza sifa zao. Hii huonyeha kwamba wapo watu wanaoabudu, lakini si waabuduji wa kweli. Wanaweza kudhani kwamba wanamwabudu Mungu lakini ukweli si hivyo maana hawatimizi masharti Yake.

Yesu alitangaza alama za wanaomwabudu  kwa kweli – wao huabudu “katika roho na kweli.” Basi, kinyume chake ni kwamba, waabuduji wasio wa kweli ni wale wenye kuabudu “katika mwili na uongo. Kimwili, waabuduji wasio wa kweli wanawea kufanya matendo yote ya kuabudu, lakini ni maonyesho tu maana hayatoki katika moyo unaompenda Mungu.

Ibada ya kweli kwa Mungu inatoka katika moyo unaompenda Mungu tu. Basi, kuabudu si kitu tunachofanya wakati tunapokutanika kanisani, bali ni kitu tunachofanya kila dakika ya maisha yetu, tunapotii amri za Kristo.

Inashangaza kwamba yule mwanamke aliyekuwa anazungumza na Yesu alikuwa ameolewa mara tano, na wakati huo alikuwa anaishi na mwanamume, na bado alitaka kuhojiana na Yesu kuhusu mahali panapofaa kumwabudu Mungu! Yeye ni mfano wa watu wengi sana wenye dini, wanaohudhuria ibada huku wakiishi maisha yao kila siku katika kumwasi Mungu. Hao si waabuduji wa kweli.

Wakati fulani Yesu aliwakemea Mafarisayo na waandishi kwa sababu ya ibada yao ya uongo, isiyotoka moyoni.

Enyi wanafiki! Ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo; ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu’ (Mathayo 15:7-9. Maneno mepesi kukazia).

Ingawa Wayahudi na Wasamaria katika siku za Yesu walitilia mkazo sana kuhusu mahali pa watu kuabudia, Yesu alisema kwamba mahali hapakuwa na maana sana. Cha muhimu ni hali ya moyo wa kila mtu, na jinsi anavyomheshimu Mungu. Hayo ndiyo yanaamua jinsi ibada yake ilivyo.

“Ibada” nyingi katika makanisa siku hizi ni taratibu tu zilizokufa, zinazotendwa na waabuduji waliokufa pia. Watu wanarudia maneno ya mtu mwingine kuhusu Mungu, bila hata kuyafikiri, wanapoimba “nyimbo za kuabudu.” Kuabudu kwao ni bure, maana maisha yao yanaonyesha kilicho halisi katika mioyo yao.

Mungu angetamani hata kuambiwa “Nakupenda” rahisi tu itokayo moyoni kutoka kwa mtoto wake mmoja mtiifu, kuliko kuvumilia kelele zisizotoka moyoni za maelfu ya Wakristo wa Jumapili asubuhi, wakiimba “Jinsi Wewe Ulivyo Mkuu.”

No comments:

© 2013 HEKIMA KWAYA MORAVIAN-KINONDONI . All rights resevered. Designed by Templateism