AD (728x90)

Tuesday, June 21, 2011

Nyota wa kwaya ya Mabalozi wa Yesu walivyozimika Tanzania

SI jambo la ajabu kupita katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam na kusikia nyimbo za kwaya ya The Ambassadors of Christ zikipigwa. Nyimbo kama 'Kwetu Pazuri', 'Kazi Tufanye' na nyinginezo huburudisha masikio ya watu kiasi cha kutafuta CD za kwaya husika.


Kwaya hiyo imepata umaarufu jijini Dar es Salaam na katika mikoa mingine kutokana na mpangilio wa sauti pamoja na ujumbe wao. Lakini ni watu wangapi wanafahamu mkasa mzito ulioipata kwaya hiyo ya Kigali, Rwanda kwenye ardhi ya Tanzania?

Hakika wapenzi wa muziki wa injili wa Dar es Salaam na hasa wale wa Kigali, Rwanda kamwe hawatasahau msiba mkubwa uliotokea Kahama, Shinyanga baada ya kwaya hiyo ya Kanisa la Sabato la Remera kupata ajali mbaya iliyochukua roho za wanakwaya watatu.

Ajali hiyo si tu kwamba iliwahuzunisha watu wa Rwanda na Tanzania pekee, bali Afrika Mashariki yote.

Makala hii inaelezea safari ya kwaya hiyo nchini Tanzania na namna walivyopata ajali.

Safari ya Tanzania
Mei 5, 2011 kwaya hiyo ilikuwa na ratiba ya kuja Tanzania ikitokea Kigali. Kwaya hiyo ilikuja Dar es Salaam kuzindua albamu ya pili ya 'Mnazorayo' huku wenyeji wakiwa kwaya ya Acacia Singers ya Kanisa la Sabato la Mwenge, Dar es Salaam.

Iliwasili Dar es Salaam, Mei 6 ikiwa salama na Mei 7 ilijiweka sawa kwa ajili ya kutumbuiza siku iliyofuata.Siku hiyo waimbaji walihojiwa 'live' katika kipindi cha 'Lulu za Injili" cha Redio Tanzania na walisikika wakiwa na furaha.

Siku ya onyesho
Mei 8 ilikuwa siku ambayo watu wengi walikuwa wakiisubiri, wakazi wengi wa Dar es Salaam na vitongoji vyake walifika katika Ukumbi wa PTA na kuangalia namna Mungu alivyoinuliwa.Kwaya mbalimbali za Tanzania zikiongozwa na  Voice of Victoy, Triumph Generation na Harvesters zilitumbuiza. Ukumbi ulijaa kiasi kwamba watu walikosa mahali pa kukaa.

Watu walilipuka kwa furaha wakati kwaya ya  Ambassadors of Christ ilipopanda jukwaani.  
Nyimbo za 'Kazi Tufanye', 'Yesu Ndiye Njia', 'Twapaona', 'Kuna Siku', 'Twatamani Kufika Msalabani' na 'Kwetu Pazuri' zilitikisa katika ukumbi huo. Baada ya tamasha, kwaya iliondoka kujiandaa kwa safari ya kurudi kwao Kigali. 

Ajali ilivyotokea
Mei 9 kwaya ilianza safari ya kurudi Kigali, Rwanda. Safari ilikuwa nzuri lakini majira ya saa 3:00 usiku hali ilikuwa mbaya. Walipofika maeneo ya Kahama, Shinyanga walipata ajali mbaya baada ya kugongana na lori.
Kwanza dereva aliona lori likiwa limeharibika barabarani na alipojaribu kulipita ndipo alikutana na lori jingine na kugongana nalo uso kwa macho.

Waliofariki
Amos Fares, Mtanzania pekee katika kwaya hiyo ambaye alikuwa amekaa kiti cha mbele, alifariki. Mwingine aliyepoteza maisha ni Filbert Manzi  ambaye pia alikuwa mtangazaji wa Redio Kigali na Mkurugenzi Ephraim ambaye pia ni mwanzilishi wa kundi. Watu wengine wanne waliumia.

Msaada wa serikali
Serikali ya Rwanda ilituma helikopta na magari kwa ajili ya kuchukua majeruhi na kutoa usafiri kwa wahanga. Amos alizikwa nyumbani kwao Kigoma wakati uku Ephraem na Filbert walizikwa Kigali, Rwanda, Mei 12.  
  
Historia ya kwaya
Kwaya ya Ambassadors of Christ ilianzishwa mwaka 1995, miaka michache baada ya mauaji ya halaiki ambapo ilikadiriwa watu zaidi ya milioni moja waliuawa.

Wanakwaya wengi walirudi Rwanda wakitokea Uganda ambako walikuwa wamekimbilia wakati wa machafuko hayo ya kisiasa.Kwaya ilianza ikiwa na watu 10 katika Kanisa la Sabato la Remera, sasa kwaya ina jumla ya watu 50.
Mungu awarehemu marehemu na awabariki waliobakia.

2 comments:

MADUHU said...

Asante kwa Taarifa hii imenikumbusha mbali leo japo Kipindi cha Lulu za Injili ni cha Morning Star Radio na sio Radio Tanzania

Unknown said...

NÃO É FACIL PERDER UM FAMILIAR OU UM AMIGO,MAIS Á NOSSA ESPERANÇA UM DIA NOS REENCONTRAR.NÃO CONHECIA, SOU BRAZILEIRO MAIS SOMOS TODOS IRMÃOS.

© 2013 HEKIMA KWAYA MORAVIAN-KINONDONI . All rights resevered. Designed by Templateism